UCHAKACHUAJI WAGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI, KANSA NYINGINE INAYOITAFUNA CCM.
Na Godfrey Mushi
WAKATI wa viongozi kuwazungusha na kuwahadaa wananchi kutokana na maamuzi yao katika michakato mbalimbali mara zinapotokea nafasi za kuwania nyadhifa kadhaa za uongozi,
iwe kupitia vyama vya siasa au sehemu ya serikali ni vyema ufikie kikomo kwa mantiki ya kuponya kirusi cha kansa kinachokitafuna Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa.
Kauli zao,vitendo vyao na misimamo yao ni kama vimenaswa na kuhifadhiwa katika njia mbalimbali za mawasiliano.
Wananchi wa sasa wameamka,wanajua kinachoendelea dhidi ya uchakachuaji, wameonyesha uthubutu kwa kuwagomea kwa kufanya maamuzi magumu, hakika wanaoendekeza ubazazi huo, kamwe hawawezi kuzuia. ni vyema waseme kweli wakati wote.
Tangu ulipoanza mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu uliomalizika mwishoni mwa mweziOktoba,wagombea mbalimbali wamekuwa wakilalamika na kupaza sauti baada ya kuchakachuliwa kwa madai ya kigezo cha ukabila,udini na makundi.
Waliothubutu kujitokeza kuwania nafasi za ubunge na hata udiwani ambao walifanya hivyo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania ibara ya 8 kifungu cha kwanza cha sheria ya mwaka 1984 ambayo inasema kuwa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii,hawajaridhishwa na maamuzi yaliyofikiwa.
Sasa hivi gumzo katika vyombo vya habari na huko mitaani ni kuhusiana na mchezo mchafu wa uchakachuaji wa majina ya waliojitokeza kuwania kuteuliwa kugombea nafazi za U-meya,Wenyeviti wa Halmashauri na manaibu wao.
Baada ya wengi wao kubaini kwamba majina yao yalianza kuchakachuliwa kwa kuwekewa alama ndogo (dhaifu) katika ngazi za Wilaya hata kabla ya kupelekwa mkoani ambako njama za kuhakikisha hawafiki kokote zilitekelezwa kwa lengo la kuwakata makali,sasa zimegeuka kidonda kilichoanza kuota uvundo.
Njama hizo za kuwafifisha wanaooneka kuwa na nguvu kisiasa, zilitengenezwa hata kabla ya majina ya wagombea kufikishwa katika kikao cha Kamati ya Halmashuri Kuu ya CCM iliyokutana Desemba 10 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo (CC) ilikutana kwa ajili ya kujadili na kutoa maamuzi ya mwisho baada ya kupokea mapendekezo yaliyofikiwa katika ngazi za wilaya na mikoa.
Lakini katika hili la uchakachuaji nani alaumiwe kati ya kamati kuu na ngazi za Wilaya na Mikoa ambazo zilidanganya kwa kuchakachua taarifa au majina ya wagombea ambayo hayakufika kamati kuu na hata hayo yaliyopelekwa na kurejeshwa tayari kwa ajili ya kupigiwa kura yapo ambayo yamegubikwa na dosari nyingi kutokana na udanganyifu uliofanywa katika ngazi za Wilaya na Mkoa.
Nimekuwa nikijiuliza mara nyingi ili kumaliza mkanganyiko na malalamiko haya ama pengine kuepusha migogoro ndani ya CCM ni kwa nini wajumbe wa Kamati kuu wanapopitia majina na mapendekezo toka mikoani, wasiangalie ama kuhoji iwapi mihutasari ya vikao vya ngazi hizo?
Kama viongozi waandamizi wa CCM wakibaini mapungufu hayo na kuwa wakali katika ukaguzi wa taarifa hasa mihutasari ya vikao vya kamati za siasa mikoani na Wilayani, ugonjwa huu wa saratani inayoitafuna CCM mithili ya siafu unaweza kutibu majeraha walao ya uchaguzi wa mameya,wenyeviti wa Halmashauri na manaibu wao.
Hakika,hiki ndicho kilichowasukuma baadhi ya wagombea wa nafasi za Umeya,Wenyeviti wa Halmashauri na manaibu wao ambao wamechakachuliwa,kuamua kujiandaa kukabiliana na fedheha ya kushindwa kwao kutokana na kigezo cha ukabila ama udini.
Tayari maamuzi magumu yaliyotokana na mchujo huo, yameleta kizaa zaa na Madiwani wengine ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wametangaza kujiuzulu nyadhifa zao kutokana na mpasuko uliopo.
Mifano anuai ya waliochukua maamuzi magumu ni pamoja na madiwani wawili wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara (CCM), Ongujo Wakibara kutoka Kata ya Mkoma na Lukio Ambogo ambaye ni diwani wa Kata ya Nyahongo.
Hawa wamelazimika kutangaza dhamira yao ya kuamua kuachia ngazi baada ya madiwani wenzao Charles Ochele,Yamo Odemba na Ongujo Wakibara, majina yao kukatwa na Kamati ya Siasa ya mkoa wa Mara.
Sakata hilo limetokea wiki chache tu baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Pius Msekwa kufika Rorya na kusikiliza malalamiko ya madiwani wapatao 10 waliokuwa wametishia kujiuzulu uanachama baada ya majina ya wagombea wenzao ambao wanatakiwa na wananchi kwa sasa kupigwa chini.
Wamefikia hatua hiyo kutokana na mpasuko wa kisiasa uliopo Wilayani humo lakini kubwa zaidi ni kutoridhishwa na mchakato mzima wa kuchuja majina kwa maana ya kuwapa alama,kutoa mapendekezo na kuainisha vigezo kadhaa ikiwemo uadilifu, na namna ambavyo wamekitumikia chama chao.
Waliochukizwa na maamuzi hayo na kutangaza kujiuzulu wakipinga majina yao kuondolewa au kukatwa kwa misingi ya kuwalinda waliokuwepo katika madaraka hayo ya Umeya,Uenyekiti au Unaibu katika nafasi hizo nyeti ndani ya Halmashauri,ndio watakaorutubisha kirusi hicho cha Saratani kinachoitafuna CCM kama dhana ya ukweli ndani ya chama hicho itafunikwa.
Yapo madai ya baadhi ya viongozi wa CCM Wilaya ya Mbeya mjini kudaiwa kuongeza mpasuko wa kisiasa katika vita ya kumpata mgombea Umeya baada ya kudaiwa kuitisha mkutano wa kuwatisha madiwani wanaoonekana kuwa na dhamira ya kukisaliti chama kwa minajili ya kushawishi upigaji kura za maruhani.
Vivyo hivyo,mgongano wenye taswira ya namna hiyo umeripotiwa ndani ya CCM Wilaya ya Morogoro Mjini ambapo baadhi ya wagombea wamelalamikia kuhujumiwa katika vita hiyo na baadhi ya viongozi wa chama ngazi ya Wilaya.
Mambo kama hayo yametokea pia huko Iringa mjini ambako majina ya madiwani waliokuwa na nguvu kisiasa na waliokuwa wakitajwa tajwa mara kadhaa kwamba wanaweza kuwa sehemu ya mabadiliko, Mussa Wanguvu na Vitus Mushi majina yao yalikatwa.
Huko Tanga nako mambo hayakuwa shwari kwani Telesphori Chambo aliyekuwa akiwania nafasi ya Umeya alienguliwa kwa itikadi zinazohusishwa na udini.
Pengine naweza kusema ‘Uchakachuaji huu wa aina yake ni kirusi cha saratani kinachoitafuna CCM taratibu na walio madarakani wasipofikiri kwa haraka kukichoma kidudu hicho, watakaribisha kura za maruhani ambazo zitaiangamiza kwa kuigharumu zaidi muda mfupi ujao’.
Cha kushangaza,badala ya kutafuta mwarobaini wa kutibu kirusi hicho cha saratani kinachoitafuna CCM hivi sasa, Katibu mkuu wa CCM Taifa Yusuph Makamba amekaririwa akisema kuwa, uamuzi wa kugombea ulikuwa hiari yao na kujiuzulu pia ilikuwa ni hiari yao na kwamba CCM haita tetereka kwa uamuzi huo.
Kauli ya Makamba inakwenda sambamba na katiba ya chama hicho ambayo inasema wazi kwamba “mtu atakoma kuwa kiongozi kwa kujiuzulu kwa hiari yake mwenyewe ama kwa kufukuzwa”.
Waswahili wanasema, ‘msafara wa nyoka hauna eskoti’…hivyo ni dhahiri kuwa wanaoendekeza dhamira katili ya kuwachakachua wenzao wasipate madaraka,hatuwaungi mkono wala kushabikia misimamo yao .
Ifike mahali,tutafakari kadhia hii ya uchakachuaji hadi lini? na ni nani angependa afanyiwe hivyo?
Godfrey Mushi ni Mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Iringa,anapatikana kwa simu namba 0767 535490 au barua pepe, ghandsome79@hotmail.com
MWISHO.