Friday, December 10, 2010

Vita ya Umeya yafunika nchi

Vita ya Umeya yafunika nchi

8th December 2010

Majeraha ya kura za maoni yaliyokigharimu Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu uliopita huenda yakakiumiza zaidi katika hatua ya kusaka mameya, naibu meya na wenyeviti wa halmashauri nchini, kutokana na makundi kuibuka tena kwenye harakati za kuwania nafasi hizo.

Kuna kampeni za kidini na kikabila zinazofanyika chini kwa chini kwa wagombea kuchafuana kwa nia ya kujiweka kwenye nafasi nzuri ya uteuzi.

Katika Manispaa ya Iringa Mjini, kama uongozi hautafunika kombe ‘mwanaharamu’ apite, vita ya makundi na ukabila katika kumpata kiongozi huyo itazidi kukimega chama hicho.
Hadi sasa vigogo watano wamejitokeza kuwania nafasi hiyo akiwemo meya aliyemaliza muda wake, Amani Mwamwindi (Mlandege), Vitus Mushi (Mtwivila), Alphonce Mlagala (Ruaha), Mussa Wanguvu (Kihesa) na Daudi Albert (Mshindo).
Vigogo hao ndio wanasaka ridhaa ya chama chao kuwa meya wa Iringa Mjini.

Kinyang’anyiro kikali kipo kati ya Meya anayemaliza muda wake Amani Mwamwindi, Vitus Mushi aliyewahi kushika nafasi hiyo. Mushi pia alipata kuwa Mwenyekiti wa UVCCM mkoa huo miaka ya nyuma.
Kwa upande wa Manaibu Meya wamo Abubakar Mtamike (Gangilonga), Ally Mbata (Kitwiru) na Gervas Ndaki (Ilala).

Baadhi ya wananchi na wadau mbalimbali wametoa hadhari kwa CCM juu ya uteuzi wa atakayegombea nafasi ya umeya kuwa kama umakini hautatawala yale ya kwenye mpasuko wa kura za maoni kwenye kuwania ubunge wa Iringa Mjini yanaweza kujirudia.

Wana CCM na wadau mbalimbali mjini Iringa, wanasema wanataka meya atakayekuwa na uwezo wa kusimamia miradi ya maendeleo kwa kasi kubwa, kuandaa mipango ya kuiwezesha Manispaa ya Iringa kuwa Jiji, kuboresha miundombinu na kumaliza migogoro ya ardhi.
“Chama kinatakiwa kiwe makini sana katika kupitia uteuzi wa majina ya madiwani waliojitokeza kuwania kiti cha u-meya, kwa kuwa tunataka meya atakayetuandaa kuwa Jiji baadaye na mwenye maono ya mbali kimaendeleo, lakini pia mwenye nia thabiti ya kuibadili Iringa kimantiki, fursa za kiuchumi na hata ukuaji wake…hapa wakikosea tena ndio itakuwa maumivu makubwa,” anasema mmoja wa makada wa CCM mjini hapa.
Kumekuwepo na hisia za ukabila na udini mjini na sasa baadhi ya waliojitokeza wamefikia hatua ya kuchafuana kwa kutengenezeana majungu ili kumdhoofisha mpinzani wake asiteuliwe kugombea nafasi hiyo.
Hali ni hiyo karibu mikoa yote ambako watu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni wenye majina makubwa na uwezo kifedha, maarufu na wale wa kawaida ambao hawavumi sana kwenye nyanja ya siasa.

Tayari Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ametahadharisha kwamba wanachama wao wenye tuhuma hawatakuwa na nafasi katika kinyang’anyiro hicho.

Hata hivyo, wapo madiwani waliowahi kuwa mameya, manaibu meya na wenyeviti wa halmashauri ambao walituhumiwa kwa kujihusisha na ulaji rushwa wamechukua fomu kuomba tena kuchaguliwa kwa mara nyingine.
Baadhi yao waliwahi kutuhumiwa katika kashfa za uuzaji maeneo ya wazi, kuingia mikataba feki ya tenda za manispaa na halmashauri, pia wamechukua fomu za kuomba kugombea nafasi walizowahi kuwa nazo.
Katika Manispaa ya Musoma Mjini, Chadema kilikuwa kimejihakikishia ushindi mapema baada ya kutwaa kata nane kati ya 13 za Manispaa hiyo, na tayari kimetwaa nafasi ya meya na naibu meya baada ya diwani wa Nyamatare, Alex Malima Kifurura kupita bila kupingwa katika nafasi ya umeya wakati naibu wake, Angela Dereki wa Kata ya Kamnyonge naye amepita.

Mbunge wa jimbo hilo, Vincent Nyerere, alisema kwamba wanachosubiri wateule hao ni kuapishwa Desemba 17 mwaka huu kama madiwani ili waanze kutekeleza sera za chama chao.
Jijini Dar es Salaam, katika Manispaa ya Kinondoni, madiwani 20 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM.

Miongoni mwa wagombea hao yupo Mkurugenzi wa Michezo ya Kubahatisha, Abbas Tarimba na Julian Martin Bujugo ambaye katika Baraza lililopita alipigania sana maeneo ya wazi kwa kutaka yasiuzwe na mwingine ni Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Songoro Mnyonge na Ibrahim Kisoky.
Wengine ni Issa Mtemvu, Charles Mgonja, Othman Kipeta, Christine Kirigiti, Majimasafi Shariff, John Mome Moro, Clement Boko, Yusuph Mwenda, Richard Chengula na Boniface Mnyachibwe.
Nafasi ya naibu meya inawaniwa na watu saba kati ya hao 20, akiwemo Rogate Mbowe, Husna Hemed na Charles Mgonja.
Katika Manispaa ya Ilala, pia mpambano ni mkali kwani wamejitosa aliyekuwa Naibu Meya katika baraza lililopita, Jerry Silaa (Ukonga), aliyekuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk. Didas Massaburi (Kivukoni) na Hashimu Saggaf (Kariakoo).

Wagombea hawa ni kama wote wananguvu kisiasa kutokana na uzoefu na nafasi ambazo waliwahi kuzishika.
Temeke nako kuna mtindo wa kuchafuana ambapo baadhi ya wagombea wametuhumiana kugawa rushwa kwa viongozi wa CCM Wilaya na mkoa.

Suala hilo limeibua mpasuko, lakini tayari kuna taarifa kwamba waliotoa taarifa hizo kwa kuandika barua kwa Makamba pamoja na watuhimiwa, watahojiwa na Kamati Kuu ya CCM.
Wanaowania nafasi ya umeya wa Temeke ni tisa; ambao ni Anderson Charles (Kijichi), Hamis Msombo (Temeke), Noel Kipangule (Chang’ombe), Zena Mgaya (Tandika), Kenni Makinda (Vituka); huyu ni kaka wa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Wengine ni Hamis Kinyaka (Mtoni), Warda Hoja (Pemba Mnazi) na Francis Mtawa (Keko).
Mkoani Mbeya, CCM kamati ya siasa imependekeza majina matatu likiwemo la meya anayetetea nafasi hiyo, ambaye pia ni diwani wa Majengo, Athanas Kapunga, Dorr Issa Mohamed (Isanga) na Juma Simbeyange wa Kata ya Nsonho.
Chadema kimemsimamisha diwani wa Kata ya Forest, Boyd Mwabulanga, kuwania nafasi ya umeya wakati Diwani wa kata ya Ruanda Albert Hubert atawania nafasi ya Naibu Meya.

Mkoani Lindi waliojitokeza kwa tiketi ya CCM ni Frank Raphael Magali (Msinjahili), Suleiman Namkoma (Matopeni), Mohamed Lihumbo (Rahaleo) na Saidi Juma (Mbanja).­­­

Wanaowania unaibu meya ni Jamaldin Mandoa (Mingoyo) na Ismail Omary Mandambwe (Tandangongoro).
Kwa upande wa CUF aliyejitokeza ni Abdallah Mohd Khatau.

Katika Wilaya ya Nachingwea, wagombea wamejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri kwa tiketi ya CCM ni Chikawe Abdallah Mussa, Mpoyo Faida Kaisi, Mbinga Abdallah Mussa, Ngatupa Hamis Mohamed, Penengu Rabia, Juma Raphael na Saanane Petro. Umakamu wa mwenyekiti ni Salima Chiwalo Hassan.
Liwale wagombea watatu wamejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ambao ni Abbas Matulilo, Hassan Myao na Mussa Omary Mkoyage.
Ruangwa waliojitokeza kuwania uenyekiti ni Ibrahim Ndoro, Beda Mbilla, Andrew Chikongwe, Litimbi Abdallah, Mussa Mtejela na Issa Libaba huku nafasi ya umakamu ikiwaniwa na Omary Songea, Mosses Mpwapwa na Fabian Nguli.
Lindi Vijijini waliojitokeza ni Makwinya Mathey Benino, Meinrad Mussa Ngombo, Rutamba na Mbonde Mussa Ahmaid Wilayani Kilwa waliojitokeza ni Ally Mohamed Mtopa anatetea kiti chake.

Moshi Mjini, Chadema kimewateua diwani wa Bomambuzi, Jaffary Michael, kuwania umeya wa Manispaa ya Moshi na diwani wa kata ya Kiborlon,Vicent Rimoi, kuwania unaibu meya.

No comments:

Post a Comment