Thursday, November 18, 2010

Anguko la mawaziri, wakuu wa mikoa funzo kwa wabunge

Anguko la mawaziri, wakuu wa mikoa funzo kwa wabunge

Na Godfrey Mushi
Kuna mwana diplomasia mmoja hapa nchini, aliwahi kusema, namnukuu; “kama wewe hauhitaji mabadiliko, basi ujue wewe ni mwathirika wa mabadiliko.”

Dhana ya mwanadiplomasia huyo inaweza kufanana na fikra nyingine kwamba, viongozi wa umma ni mfano wa marubani…hawaruhusiwi kubeba abiria bila kufuzu.

Rubani anapofikia hatua ya kurusha ndege angani, hawezi kusahau kwamba upo wakati atalazimika kutua ardhini, iwe ni kutokana na kuishiwa mafuta, hitilafu au kutua kwa usalama.

Ndivyo ninavyoweza kuzungumzia anguko la baadhi ya `vigogo’ wa siasa waliokuwa katika nyadhifa za uwaziri na ukuu wa mikoa, lakini wakashindwa kutetea ubunge wao.

Lakini wapo `vigogo’ wengine waliokuwa maarufu sana katika siasa za nchi hii. Hawakuwa mawaziri ama wakuu wa mikoa. Lakini wameshindwa vibaya. Wameanguka katika kuwania ubunge.

Zipo sababu nyingi zinazotajwa kuwa chanzo cha anguko la `vigogo’ hao, lakini kwa ujumla wake, hatua hiyo inaonekana dhahiri kuwa ni viashiria vinavyothibitisha kujisahau kwao, kusahau wajibu wao hasa kwa wapiga kura katika kipindi walipokuwa wabunge.

Waliposhika nyadhifa za juu ama kupata umaarufu wa kisiasa, wakasahahu kwamba asili yake ni wananchi walio katika mahitaji ya kuvushwa salama kutoka katika umasikini unaowakabili na kwenda katika ustawi bora wa maisha.

Walishindwa (tena inawezekana ni kutokana na uzembe ama dharau), kurejea kwa wananchi, kukaa na wapiga kura wao, kuzungumza nao, kupanga na kushirikishana namna bora ya kujiletea maendeleo.

Hawakurudi kwa wananchi ili kueleza mambo mema waliyoyafanya na changamoto zilizowakabili. Wakajiona na kuamini kwamba `wao ndio wao’.

Kana kwamba haitoshi, inawezekana waliendelea kuota njozi, kuwa watadumu katika uongozi wa umma mpaka watakapoitwa na Mwenyenzi Mungu.

Umma umewashuhudia `vigogo’ wakishindwa kunadi sera za chama tawala-Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichowateua kwa kuwaamini, kwamba wangekipatia ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Zipo taarifa na vielelezo vinavyothibitisha jinsi miongoni mwa `vigogo’ hao waliposhindwa kuzinadi sera na ilani ya CCM, badala yake wakaendeleza mashambulizi binafsi na kashfa dhidi ya wagombea wengine.


Hakika, anguko la `vigogo’ wa CCM na kufufuka kwa upinzani nchini, kumetokana na wananchi kuchoshwa na ubabaishaji wa baadhi ya viongozi ndani ya CCM na serikali yake, kutofikiwa kwa matarajio ya umma, kushamiri kwa ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Hadi sasa wapinzani wameweza kusonga mbele na kunyakua majimbo mengi zaidi kuliko ilivyokuwa tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, 1992.

Inashangaza kuona wapo baadhi ya watu wasiokubali kuwepo kwa mabadiliko hayo. Watu wa aina hiyo wanaamini kwamba ikiwa upinzani utashinda na kutwaa madaraka, kuna uwezekano wa kutokea machafuko.

Na wapo wengine wanaoamini kwamba asipochaguliwa mgombea ubunge kupitia CCM, eneo la jimbo husika litatengwa na serikali na kukosa miradi ya maendeleo na ustawi wa jamii.

Ilitarajiwa kwamba wagombea wakiwemo `vigogo’ walioangushwa, wangejikita zaidi katika kuelezea sera, ilani za vyama vyao na kutoa taarifa sahihi ya utekelezaji wa ahadi za kipindi kilichopita.

Lakini walizigeuza kampeni kuwa sehemu ya kufanya siasa za kuzungumzia maslahi binafsi na kuchukua muda mwingi kuwatuhumu waliojitokeza kidemokrasia kupambana nao.

Hata hivyo, baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu katika nafasi mbalimbali za uongozi wa kuchaguliwa, iwe urais, ubunge, udiwani ama ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ni wakati wa kukaa na kutafakari changamoto zilizojitokeza na kuchangia kushindwa kwao, ikiwezekana kujipanga upya.


Mkoani Iringa

Lakini katika mkoa wa Iringa, tulishuhudia majimbo matatu kati ya 11 `yakiwaka moto’ kutokana na kiwango kikubwa cha ushindani wa kisiasa wakati wa kampeni.

Hali ilisababisha kuibuka kwa utabiri usiokuwa rasmi, kwamba kutakuwa na anguko kubwa la `vigogo’ waliokuwa wakitetea nafasi zao za ubunge.

Majimbo hayo ni Njombe Magharibi lililokuwa na mgombea wa CCM, Gerson Lwenge (kwa sasa mbunge mteule) aliyeshinda kwa kura 29,743 dhidi ya Thomas Nyimbo wa Chadema aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura 13,483.

Majimbo mengine ni Njombe Kaskazini ambalo lilikuwa na mgombea wa Chadema, Alatanga Nyagawa na Deo Sanga ambaye kwa sasa ni mbunge mteule na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa.

Licha ya CCM kupata ushindi katika majimbo hayo, lakini upepo wa mabadiliko ulishamirisha ushindani hadi katika majimbo ambayo `vigogo’ wa chama tawala walianguka.

Hali hiyo ilionekana katika majimbo kama la Iringa Mjini ambalo lilikuwa na wagombea wa vyama vitatu vya siasa, akiwemo Mbega wa ambaye pamoja na Mariam Mwakingwe wa NCCR-Mageuzi,walishindwa na Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.

Zipo sababu nyingi zilizotolewa kuhusu kutokukubalika kwa Mbega, mojawapo ikiwemo ni kutoonekana jimboni kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Mbega alijitetea mara kadhaa kwamba kasoro hiyo na nyingine zilizoelekezwa kwake, zilitokana na kuangushwa na wasaidizi wake, aliowaacha jimboni humo, lakini wakashindwa kutekeleza wajibu wao.

Monica, aliangushwa baada ya Mchungaji Msigwa kupata kura 17,742 kati ya kura 35,910 zilizopigwa, huku Mbega akiambulia kura 16,916 na Mwakingwe akipata kura 950.

Iringa Mjini ni sehemu moja ya majimbo yaliyoshuhudia `vigogo’ wakiangushwa katika nafasi za ubunge.

Imedhirika kwamba hivi sasa kuna wapiga kura wasiokubali kuyumbishwa katika kufikia uamuzi unaokidhi maslahi ya umma.

Mathalani Wahehe wana desturi ya kutumia msemo unaosema, ‘nene swela’, yaani ‘mimi basi’, wakiwa na maana kwamba hawakubaliani na mtu fulani, lakini hapo unaweza kuwa nao na wasikuonyeshe kama wanafikiria kutumia neno hilo mbele yako.

Majimbo mengi likiwemo la Iringa Mjini yana wapiga kura wenye tabia ya kubadili viongozi wa kuchaguliwa bila kujali vyama wanavyotoka, ili mradi wanabaini kwamba kiongozi aliyepo hakidhi matarajio yao.

Mathalani, mwaka 1995 Iringa Mjini lilichukuliwa na wapinzani kama ilivyo sasa, likiwa chini ya Faramagoha Kibasa aliyekuwa NCCR-Mageuzi.

Ushindi huo ulipatikana dhidi ya Hans Kitine, bosi wa zamani wa usalama wa taifa, aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CCM.

Vivyo hivyo safari hii imekuwa ni zamu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuliwakilisha jimbo hilo, baada ya kuwashinda wapinzani wake akiwemo Mbega wa CCM.
Changamoto kwa washindi

Wanasiasa waliowaangusha `vigogo’ katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, wanapaswa kubaini kwamba mahitaji na matarajio ya umma kwa wabunge wao bado yapo.

Kwa kadri walivyokuwa wanahitaji kutoka kwa `vigogo’ hao, ndivyo watakavyohitaji kutoka kwao na kwamba wasipotimiza matakwa hayo, wasitegemee kuikwepa adhabu iliyowapata `vigogo’ husika.

Mfano halisi umeonekana katika jimbo la Iringa Mjini katika kipindi cha kuanzia Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995.

Katika kipindi hicho, wapiga kura wameshawachagua wabunge kutoka vyama vya NCCR-Mageuzi, CCM na sasa Chadema.

Wanapaswa kuyatambua makundi mbalimbali ya kijamii hasa wanawake na vijana walioshiriki kikamilifu kuwapigia na kulinda kura kiasi cha kufanikisha ushindi walioupata.

Zipo ahadi kadhaa zilizotolewa na washindi, miongoni mwa hizo zikiwa ndani ya ilani za vyama vyao na nyingine zikitokana na mahitaji ya papo kwa hapo.

Zote hizo zinastahili kuwekwa katika kumbukumbu na kutekelezwa, kama ilivyokuwa kwa Mchungaji Msiwa alipoahidi, kwamba baada ya kuapishwa na kuanza kazi ya uwakilishi bungeni, ataweka Mwanasheria katika ofisi yake, ili ashughulikie matatizo mbalimbali ya wananchi.

Ahadi nyingine ilikuwa ni kushirikiana na uongozi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa, kutatua matatizo ya ardhi, upimaji wa viwanja, kuongeza na kupanua huduma za ughani kwa jamii ya wafugaji, wakulima na kufufua sekta ya utalii.

No comments:

Post a Comment