Thursday, November 18, 2010

WATU ZAIDI YA 90,000 IRINGA NI MBUMBUMBU WASIOJUA KUSOMA WALA KUANDIKA

WATU ZAIDI YA 90,000 IRINGA NI MBUMBUMBU WASIOJUA KUSOMA WALA KUANDIKA

Na Godfrey Mushi.

SERIKALI tayari imetangaza kwamba inakusudia kuifanya elimu ya kidato cha nne kuwa elimu ya lazima kwa kila mtanzania.

Ni mpango mzuri kwa ujenzi na ustawi wa taifa letu ambao kimsingi umelenga kumfanya kila mtanzania kupata elimu hiyo badala ya ile ya msingi ambayo huanzia darasa la kwanza hadi la saba.

Lakini ninachojiuliza kwa sasa ni kwamba, wakati tunapiga hatua hiyo, hivi ni wenzetu wangapi ambao hata hiyo elimu ya msingi hawakuipata na hawatarajii kuipata.

Nilimkariri Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Jumanne Maghembe hivi karibuni akiwa mkoani Kilimanjaro nyakati za kampeni akisema ya kuwa serikali imeamua kwamba kuanzia sasa elimu ya kidato cha nne itakuwa ya lazima.

Hakika nilistaajabu na kuhisi msisimko, ambao ulinifanya niperuzi baadhi ya kumbukumbu zangu katika mkoa mmoja tu wa Iringa kujua ni watu wangapi ambao bado ni mbumbumbu ambao hawajui kusoma,kuandika wala kuhesabu.

Niligundua serikali ilikuwa na wazo zuri kama ilivyoanzisha Shule za Sekondari za Kata ambazo kimsingi zimeonyesha mafanikio kwa kiasi fulani katika jamii yetu.

Katika mkoa wa Iringa kuna idadi ya zaidi ya watu 90,783 wasiojua kusoma,kuandika wala kuhesabu na hawatarajii kufikia kusudio la serikali ililotangaza hivi karibuni kwamba lazima elimu ya kidato cha nne iwe elimu ya lazima.

Ninafikiri serikali ingeweka pia mkazo katika kulinasua kundi hili katika umbumbumbu kwakuwa hawa nao ni wapiga kura na wamekuwa wakikosa haki zao mbalimbali au kushiriki mambo kadha wa kadha kutokana na kuona haya kwamba watashitukiwa wakienda huko maana hawajui kusoma wala kuandika.

Kwa mtazamo wangu ni lazima uwepo kwanza mkakati wa kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma, kuandika wala kuhesabu kwa kuanza kuwafundisha kilazima wananchi hawa kupitia mpango wa elimu ya watu wazima (MKEJA).

Ni lazima tuhakikishe kwamba watu hao wanaingia darasani kilazima kabla ya kutaka kila mtu awe na elimu ya kidato cha nne na zoezi hilo lihusishe wilaya zote ili kuwsaidia watu hao kuelimika kutokana na mabadiliko ya Sayansi na teknolojia.

Hakuna njia ya mkato ya kufuta ujinga zaidi ya kutumia njia aliyoianzisha hayati mwalimu, Julius Nyerere katika miaka ya 1970. Mwalimu Nyerere alihakikisha kila mwananchi asiyejua kusoma, kuandika wala kuhesabu aliingia darasani kufuta ujinga kupitia elimu ya watu wazima.

Bado kuna changamoto nyingi katika kufikia mafanikio ya mpango huo wa serikali kwakuwa mbali na mpango wa Mkeja, zaidi ya wanafunzi 1,298 wakiwemo wavulana 669 na wasichana 629 wamekosa elimu ya msingi katika umri unaostahili mkoani Iringa.

Ni vyema ukawepo mkakati wa kuhakikisha kwamba serikali inaongeza vituo kwa ajili ya wanafunzi wa MKEJA na MEMKWA ili waliokosa wapate elimu hiyo.

Utaratibu huo utakuwa ukiwasaidia wanafunzi hao kujiunga katika shule za kawaida za msingi na hivyo kuendelea na wasomo yao vizuri kama waliopo katika mpango maalumu wa shule za msingi.

No comments:

Post a Comment