Thursday, November 18, 2010

BUNGE LA 10 LIWE CHACHU YA MABADILIKO YA KATIBA NA UUNDAJI WA TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI.

BUNGE LA 10 LIWE CHACHU YA MABADILIKO YA KATIBA NA UUNDAJI WA TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI.

Na Godfrey Mushi
IDADI ndogo ya wananchi waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu pamoja na dosari nyingine zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo, hakika zimedhihirisha kwamba Tanzania tunahitaji chombo huru cha kusimamia chaguzi zetu ili kuzifanya ziwe huru na za haki.

Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) ya sasa iliyopo chini ya Jaji Lewis Makame, si huru na inaundwa na kada zinazohusisha hata watumishi wa umma ambao wanaitii serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Wapo watakaochelewa kuamini haya yanayopiganiwa na wanaharakati kuhusu kuundwa kwa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi baada ya uchaguzi mkuu wa sasa kumalizika.

Hakuna asiyetambua kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya,Miji,Manispaa na Majiji walikuwa maajenti wa NEC kama wasimamizi wa uchaguzi mkuu.

Ukiwaacha hao wamo pia Watendaji wa Kata ambao ni Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi lakini wengi wao ni makada na wakereketwa wakutupwa wa CCM, sasa tutawaaminije kwamba wanaweza kutenda haki pale chama tawala kinaongoza serikali kinaposhindwa.

Wote hawa ni watendaji wa Serikali na wanafanya kazi kwa kufuata maelekezo ya mwajiri yaani serikali iliyo chini ya chama tawala (CCM),hakika hawawezi kumwangusha aliyewaweka hapo labda NEC ivunjwe na kuundwa mpya ambayo haitahusisha watendaji wa umma.

Swali la kujiuliza ni kwamba, nani kati ya hawa wenzetu atakubali kuadhibiwa na aliyemwajiri kwa sababu maelekezo aliyopewa hakutekeleza (kuisaidia CCM ishinde)...hakika hakuna atakayebukali hilo akikumbuka kilichomnyoa kanga manyoya shingoni.

Ni wazi kwamba tunahitaji tume huru ambayo viongozi na watendaji wake, watafanya kazi zao bila ya kuhofu kupoteza kazi zao kama hawatakisaidia chama tawala kwa namna moja au nyingine.

Ipo haja ya kuundwa kwa tume hiyo ambayo watendaji wake, hawatafungwa na kitanzi cha uaminifu na uadilifu ama uwezo wao kutiliwa shaka na umma wa watanzania.

Tumeshuhudia udhaifu pale Tume ilipotangaza matokeo ya kura za Rais katika jimbo la Geita ambapo ilitangaza aliyekuwa akiwania kiti hicho kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk.Wilbrod Slaa kwamba amepata kura 3,750 badala ya kura 25,000 na ushehe hivi.

Tafsiri hii ya makosa yakutiliwa shaka inawakatisha tamaa wapiga kura na ni mojawapo ya vitu vinavyowafanya baadhi ya watu waamini kwamba NEC inatumika kuisadia CCM.

Tanzania inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 44 kwa sasa lakini kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC),waliojiandikisha kupiga kura na kushiriki uchaguzi mkuu uliopita walikuwa watu milioni 20.1 sawa na asilimia 42.

Wachache walio katika madaraka na pengine ndani ya Chama cha Mapinduzi, wanaweza wasione umuhimu wa kufanyika kwa mabadiliko haya kwakuwa wengi wao hawaguswi na hisia za umma kuhusu hoja ya kuundwa kwa tume huru.

Yupo mwanadiplomasia mmoja aliwahi kusema ‘namnukuu’ “watu wengi wanadhani kwamba kero zao zinaweza kuondoka kwa kufanya kero…lakini kero huondoka kwa kuzielewa,kuzijadili na kuzitafutia ufumbuzi tena kwa juhudi na maarifa”.

Jirani zetu Kenya, wamefanikiwa kuwa na Tume huru ya uchaguzi baada ya ile iliyokuwa ikiongozwa Samweli Kivuitu kuvunjwa baada ya kusababisha machafuko na mauaji ya raia baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Tume hiyo ilikuwa ikituhumiwa kuhusika katika uchakachuaji wa matokeo ya nafasi ya rais wa nchi hiyo kwa kumrejesha madarakani Rais wa sasa, Mwai kibaki aliyekuwa amekataliwa na Wakenya.

Si dhani kama ni busara kwa watawala wetu kusubiri yatokee kama yaliyotokea nchini Kenya ndo waone umuhimu wa kuunda tume huru ya uchaguzi.

Ni vizuri tukajipanga sasa na kuanza mchakato wa kuhakikisha kwamba Serikali ya Rais Jakaya Kikwete inachukua jukumu la kuunda tume mpya ya uchaguzi ambayo itakuwa huru.

Mathalani,vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamikia mara kadhaa Katiba ya nchi iliyopo pamoja na uteuzi wa maofisa wa tume ya taifa ya uchaguzi.

Ni jambo la busara na hekima kuona mambo haya mawili hayabinafsishwi na watawala kwa maana kwamba, tunataka yapewe uwanja mpana wa kujadiliwa na kufikiwa mwafaka na jamii yote.

Wabunge wetu tuliowachagua ni vyema wakafunga kibwebwe katika kulipigania hili la kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi pamoja na mabadiliko ya katiba, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwingine ifikapo mwaka 2015.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa hapa nchini,wasema kuwa sababu kubwa ya wananchi kutojitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita wa Oktoba 31 mwaka huu ulisababishwa na wapiga kura kufohia utendaji wa tume ya taifa ya uchaguzi ndio maana hawakujitokeza kwa wingi kama ilivyotarajiwa.

Kwa mtazamo wangu kutokana na hoja zinazotolewa na wanaharakati wakiwemo wapinzani wa Chama cha Mapinduzi ni vyema mabadiliko ya katiba yakafanyika na kuruhusu uundwaji wa tume huru ambayo haitakuwa ikilalamikiwa na kuona kama inakilinda chama tawala.

Katika hili ni busara tukaweka maslahi ya Taifa mbele kwa sababu inawezekana ikawa ni sababu mojawapo iliyowafanya wananchi wasijitokeze kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Mmoja wa wanasiasa wa siku nyingi na kada wa CCM mkoani Iringa,David Butinini aliwahi kuniambia siku moja kwamba, ili ipatikane tume huru ya uchaguzi hapa nchini,

itatulazimu kuweka mazingira ambayo yatafanya kila mtu aone kwamba ni mazingira mazuri yasiyo na shaka na kwa namna moja au nyingine, wananchi walishirikishwa kuyaandaa kwa maana ya namna ya kupata katiba mpya na jinsi ya kuchagua tume ya uchaguzi.

“Inawezekana tume ikawa ni ya watu waadilifu lakini kama taratibu za uteuzi wake zinatoa mwanya wa kutokuwa na imani nayo,basi hiyo kasoro inaweza ikafanya watu waone ni kubwa…Hivyo,kwa namna moja au nyingine inaweza ikapunguza ushiriki katika zoezi la upigaji kura za kuwachagua viongozi wetu kama tulivyoona katika uchaguzi mkuu uliopita”,anasema Butinini.

Novemba 12 mwaka huu, umma wa Watanzania ulishuhudia wabunge wateule 327 wakila kiapo katika ukumbi wa bunge mjini Dodoma baada ya wabunge kupiga kura ya kumchagua Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anna Semamba Makinda (Mbunge wa Njombe Kusini).

Makinda alishinda baada ya kuchaguliwa kwa kura 265 katika ya kura 327 zilizopigwa na kumwangusha mpinzani wake Mwanasheria mashuhuri Maberere Marando aliyepata kura 53.

Kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Spika, Makinda alisema kuwa anataka bunge la 10 liwe ni bunge moja litalalofanya kazi kwa karibu na wabunge wote kwa maslahi ya watanzania na si ya watu binafsi.

Kwa mantiki hiyo,tunategemea bunge hilo litamaliza kiu ya watanzania ya kutaka kuwepo kwa mabadiliko ya katiba ambayo itapelekea kufumiliwa kwa NEC na kuundwa kwa tume mpya ambayo itakuwa tume huru na ya haki kwa vyama vyote.

Vivyo hivyo,tunawategemea wabunge wanaounda kambi ya upinzani bungeni wakati ukifika wapenyeze hoja ya kuifumua katiba ya nchini pamoja na tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) ili iundwe mpya itakayokuwa haiteuliwi na Rais kama hii iliyopo hivi sasa.

Safari hii kambi ya upinzani bungeni inaongozwa na chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kuwa na wingi wa wabunge.ina wabunge 45 ikifuatiwa na chama cha wananchi CUF chenye wabunge 34 huku TLP na UDP vikiwa na mbunge mmoja mmoja.

Safu hiyo inaongozwa na mbunge wa Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro Freeman Mbowe na Naibu wake Zitto Kabwe,mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mnadhimu mkuu wa kambi hiyo Mwanasheria, Tundu Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki.

Hawa ni miongoni mwa askari wanaotegemewa katika mapambano dhidi ya serikali katika kuhimiza yafanyike haraka mabadiliko ya katiba yatakayotoa fursa ya kuundwa kwa tume mpya ya uchaguzi itakayo kuwa huru nay a haki ambayo haitaingiliwa utendaji wake kwa namna moja au nyingine.

Godfrey Mushi ni mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Iringa,anapatikana kwa simu namba 0715 545490 ama barua pepe, ghandsome79@hotmail.com

No comments:

Post a Comment